Riyaa (Shirki Iliyofichikana)
Abuu 'Abdillaah
بسم الله الرحمن الرحيم
Kilugha
‘Riyaa’ ni neno linalotokana na neno la Kiarabu 'ra-aa' ambalo lina
maana ya kuona, kutazama au kuangalia. Na haswa makusudio yake ni
kujionyesha, unafiki na udanganyifu. Katika mtazamo wa kisheria Riyaa
ina maana ya ‘‘kufanya matendo ambayo ni ya kumpendezesha Allaah lakini
kwa nia ya kumridhisha asiye Allaah.’’ Au ni kufanya amali njema kwa
makusudio ya kuonesha watu, ili uonekane ni mzuri au mwema kuliko
ulivyo, ama upate kupendeza machoni mwao au upate kilicho mfukoni mwao
au cheo. Na hii Riyaa ni namna ya shirki, kadhalika ni namna ya unafiki
au wizi. Hivyo basi yoyote mazuri yafanywayo kwa kutaka na kutaraji
manufaa ya kilimwengu na sio kumridhisha Muumba, basi yanageuka kuwa ni
matendo ya kishaytwaan.
Riyaa
ni moja ya mafungu ya matendo hatari mno ambayo ni vigumu sana kwa
wengi kuyachuja na kuyatenga mbali na matendo yao. Ni vizuri na muhimu
kuweza kulichunguza tatizo hili na kulijua undani wake ili tuweze
kupambana nalo na kulitibu kwa ajili ya kufikia mafanikio ya kusafisha
amali zetu na kukamilika Uislam na Uchaji Allaah wetu. Wanachuoni wa
Ahlus-Sunnah wameelekea katika Qur-aan na Sunnah sahihi pamoja na
mwelekeo wa wema waliotangulia ili kupata tiba ya ugonjwa huu hatari. Ni
muhimu kuangalia hii Riyaa ilivyo tujue madhara yake na jinsi ya
kutafuta kinga au ponya yake.
NIYYAH
Ni
muhimu sana kufahamu maana ya Ikhlaas (utii kamili, kuitakasa niyyah)
yaani kufanya jambo kwa ajili ya Allaah pekee. Hadiyth ifuatayo
yatuonyesha namna gani tunapaswa kutilia umuhimu mkubwa juu ya Ikhlaasw
na kuwa mbali na Riyaa. ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu 'anhu)
kamnukuu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika matendo yanatokana na niyyah, Na kila mtu atapata (malipo) kwa kile alichonuia …" [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd].
Na Qur-aan vilevile inaonyesha na kueleza umuhimu wa ikhlaasw pale Allaah Aliposema: {{…wala msitoe ila kwa kutafuta radhi ya Allaah…}} [Al-Baqarah: 272].
Kizazi
cha mwanzo cha Uislam kilizingatia mno umuhimu wa ikhlaas na jinsi ya
kusafisha na kuzisahihisha niyyah zao. Tunapata mfano mzuri kutoka
katika mapokezi haya ya Ibn Mas’uwd (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyoyapokea
kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ''Maneno
pekee hayana faida kama hayajafuatiwa kwa vitendo, na maneno na vitendo
pekee havina faida kama hadi yawe na niyyah safi. Na hayo maneno,
vitendo na niyyah safi, yote hayana faida hadi yawe yamekubaliana na
Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).'' Hivyo
basi, tunaona kuna mfululizo wa masharti ambayo ndiyo yanayosababisha
vitendo vikubalike na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Sharti la kwanza ni
kwamba lazima kitendo kifanywe kwa ajili ya Allaah pekee. Sharti la
pili
kitendo
hicho kiwe kimekwenda sambamba kulingana na mafunzo ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisiwe ni kitendo cha uzushi
kilichoanzishwa na watu.
HATARI AU MADHARA YA RIYAA
1. Shirki iliyofichikana
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mapenzi yake makubwa
mno kwa ummah wake alikuwa akichunga sana na kuchelea maafa kwa ummah
wake kuliko mtu mwengine yeyote. Abu Sa’iyd (Radhiya Allaahu 'anhu)
anaeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
aliwakuta wakijadiliana kuhusu Dajjaal na akawaambia: ‘‘Je,
niwajulisheni kile nikikhofiacho zaidi kwenu kuliko hata hatari za
Dajjaal? Basi ni shirki iliyojificha. Mtu anasimama kuswali, anaipamba
na kuiremba swala yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama.’’ [Sunnan Ibn Maajah, namba 3389].
2. Inadhoofisha imani na kumpwekesha Allaah
Kwa
kufanya Riyaa, mtu huwa anaiangamiza lengo kuu la uumbwaji, kwani
badala ya kumuabudu Allaah, huwa anafanya ibada lakini kwa lengo na nia
ya kuwaridhisha waja na kupata sifa kutoka kwa viumbe na wala si kwa
ajili ya Muumba. Allaah Anasema: {{Sikuwaumba majini na wana Aadam ili wapate kuniabudu}} [Adh-Dhaariyaat: 56].
Vilevile
Allaah Anawasifia wale waumini wa kweli wanaofanya matendo ya ibada zao
kikamilifu na pekee kwa ajili yake Allaah na wala hawahitaji malipo au
shukurani kutoka kwa viumbe wenzao. Anasema Allaah: {{Na
(hao waumini) huwalisha chakula maskini na mayatima na wafungwa, na
hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho). (Hujisemea wenyewe
katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho) Tunakulisheni kwa ajili ya
kutaka Wajihi wa Allaah (tu) hatutaki kwenu malipo wala shukurani}} [Al-Insaan 8-9].
Na pia kwa upande wa pili kinyume na hao Allaah Anawaelezea wengine kwa kusema: {{Basi
ole wao wale wanaoswali Swalah zao (kinafiki). Ambao wanapuuza
maamrisho ya Swalah zao. Ambao hufanya ('amali zao ili waonekane na
watu) Riyaa. Na huzuia misaada (basi Swalah zao hazina faida).}} [Al-Maa’uwn: 4-7].
3. Inazidisha upotofu
Hakuna
shaka mtu mwenye kufanya Riyaa huwa ni mwenye maradhi moyoni mwake, na
kama ugonjwa huo hautotibiwa, uatapelekea kwenye matatizo mengi zaidi.
Kulingana na hili Allaah Anasema: {{Wanajaribu
kumdanganya Allaah na wale walioamini, lakini hawadanganyi ila nafsi
zao; nao hawatambui. Nyoyoni mwao mna maradhi (ya mashaka na unafiki),
na Allaah Amewazidishia maradhi…}} [Al-Baqarah: 9-10].
4. Inapokonya baraka ya matendo
Katika
Hadiyth nyingi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
anaelezea kwamba Allaah Hapokei matendo yanayofanywa kwa ajili ya
kuwaridhisha viumbe. Amepokea Mahmuwd bin Labiyd (Radhiya Allaahu 'anhu)
kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Allaah
Mtukufu Atasema wakati Akiyahesabu matendo ya viumbe (kuwaambia
waliofanya Riyaa), ‘‘Nenda kwa wale uliokuwa ukiwaonyesha matendo yako
(duniani) uone kama utapata malipo yoyote kutoka kwao.’’ [Swahiyh at-Targhiyb wat-Tarhiyb namba 29].
5. Inamzuia mtu kwenda peponi
Kufanya
matendo mema kwa ajili ya kusifiwa na kuridhisha watu, huenda
yakapelekea kumzuia mtu kuingia peponi. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu
'anhu) amemnukuu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
akisema: "Yeyote anayechuma elimu ambayo
anapaswa kuitumia kwa ajili ya Allaah, (kisha akaitumia) kwa nia ya
kupata manufaa ya kilimwengu, hatonusa hata harufu ya pepo siku ya
Qiyaamah." [Abu Daawuwd namba 3656, na Ibn Maajah namba 255].
MAMBO YANAYOSABABISHA RIYAA KWA UJUMLA
Kiburi
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). kasema:
‘‘Kibr ni joho langu na ukubwa (utukufu) ni kanzu yangu, hivyo yeyote
anayetaka kushindana nami (katika sifa hizo), basi nitamtosa katika
Jahanam’’ [Swahiyh Muslim namba 6349].
Kisha Allaah Ameeonya vikali kwa mwenye kutumbukia katika sifa hii aliposema: {{Usidhani
wale wanaofurahia mambo (mabaya) waliyoyafanya na wakapenda kusifiwa
kwa yale wasiyoyafanya; usidhani wao watasalimika na adhabu; (hapana,
bali) itakuwa kwao adhabu iumizayo.}} [Al-‘Imraan: 188].
Kujionesha na kujisifu
Allaah Anasema katika Qur-aan: {{Hakika
wanafiki wanataka kumdanganya (hata) Allaah Atawaadhibu kwa huko
kujaribu kwao kumdanganya. Na wanaposimama kuswali, husimama kivivu (na
kichovu) na ni kuchache mno kumkumbuka kwao Allaah}} [An-Nisaa: 142].
Pia
mtu kufanya ibada kwa bidii na kuiremba na utulivu na unyenyekevu wa
hali ya juu kwa sababu kuna watu wanamuona au kumtazama, lakini anapokua
peke yake ibada ile huifanya kwa haraka haraka na kilegevu na uchovu
kama mtu aliyelazimishwa.
Ama
mtu anatoa msaada au sadaka pale anapoona watu wapo au kuna mtu ambaye
anamuheshimu au kumjali yupo hapo. Ni mfano wale tunaowaona wanapotoa
mchango au msaada wanaita waandishi wa habari na wapiga picha na
televisheni wachukue maelezo na picha wakati anapotoa ili ulimwengu wote
ujue fulani katoa na ni mtu mzuri! Ajabu, yote hayo ni kwa maslaha ya
kiulimwengu na hakuna nafasi ya Allaah ya kutiiwa na kuridhishwa. Allaah
Hakuliacha hili pia kulikemea: {{Kwa yakini
hao hawatokufaa chochote mbele ya Allaah. Na hakika madhalimu ni
marafiki wao kwa wao. Na Allaah ni rafiki wa wale wenye kumcha.}} [Al-Jaathiyah: 19].
Kumridhisha Allaah na hapo hapo huwaangushi viumbe
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ‘‘Allaah
Mtukufu Anasema: ‘‘Mimi ni mwenye kujitosheleza, sihitaji msaada wala
mshirika. Kwa hiyo, yule afanyaye kitendo kwa ajili ya kumfanyia kiumbe
(na hapo hapo anakifanya kwa ajili Yangu), (sitokihitaji kitendo chake
hicho) nitamwachia huyo aliyemfanyia kunishirikisha Nami’’ (hatopata
ujira wowote kwa kitendo hicho). [Swahiyh Muslim namba 7114].
Mavazi
Suala
la mavazi linaweza kumsababishia mtu kuingia katika Riyaa, mathalan,
utakuta mtu anavaa vizuri akishindana na kila mitindo mipya itokayo na
akitaka watu wamuone kuwa anakwenda na wakati. Na mtu mwingine akawa
anavaa ovyo ovyo (akijiweka kama hao wanaojiita madaruweshi) akionyesha
watu kuwa haijali dunia bali yeye ni wa Akhirah tu n.k. Wengine wakivaa
mavazi fulani fulani yanayoonekana ya kidini ili asemwe kuwa yeye Shaykh
au Mwanachuoni. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: {{Na
unapowaona, miili yao inakupendeza, na wanapoongea, unasikiza usemi wao
(kwa vile unavyovutia na kupendeza); lakini wao ni kama boriti
zilizotegemezwa; (kama magogo ya miti isiyo na faida); wanadhani kila
kishindo (kinachosikika) ni juu yao (kinawatafuta wao). Hao ni maadui,
jihadhari nao. Allaah Awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki!!}} [Al-Munaafiquwn: 4].
Watu
kama hao tunao katika jamii yetu, ambao kazi yao ni kutumia ulimi wao
kudanganya watu na kufitinisha baina ya Waislam, na kuwazulia watu mambo
kadha wa kadha ili wasiwe na thamani katika jamii! Na jambo la
kusikitisha zaidi ni kwamba jamii inafunika maovu yao na inashirikiana
nao na kuwapa nafasi katika mambo ya dini na uongozi.
MAMBO YENYE KUHUSISHWA NA RIYAA
Sifa zisizokusudiwa
Endapo
watu watahudhuria shughuli ya dini kama mhadhara n.k. ambapo kuna
manufaa na kunafanywa kwa Ikhlaasw, si kunafanywa kwa malengo tofauti
kama ya kujionyesha kwa watu kuwa mnaisimamia dini na hali hamna malengo
yoyote wala hamjali kinachozungumzwa hapo kinafanywa kwa ikhlaas au kwa
sifa na kutaka tu watu waseme: ‘‘jamaa wanafanya harakati maa shaa
Allaah.’’ Shughuli kama hiyo ikiwa ni ya Ikhlaasw na wasikilizaji
wakampongeza Mhadhiri, basi pongezi hizo hazitomharibia vitendo vyake
maadam hajaigeuza au kuibadili ile nia yake kutoka kwa ajili ya Allaah
na ikageuka ikawa ni kwa ajili ya wale wenye kumpongeza na kumsifu. Abu
Dharr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam). ‘‘Ee Mjumbe wa Allaah!
Je, unaonaje kama mtu anafanya matendo mazuri, kisha watu wakamsifia kwa
matendo yake? Akajibu: ‘‘Hiyo ni sehemu ya baraka na radhi kwa Muumini
(zitakazohifadhiwa kwake siku ya Qiyaamah." [Swahiyh Muslim namba 6388].
Lakini
awe makini mwenye kupongezwa au kusifiwa kwa matendo yake mazuri, kuwa
pongezi hizo anazosifiwa akiwa ni Mhadhiri, Msomaji Qur-aan au
Mdarisiji, zisije zikambadilisha nia yake na akawa kila mara anafanya
jitihada zaidi kuremba mawaidha au kisomo chake ili azidi kusifiwa na
kupata umaarufu! Kuna wengine maskini hujitahidi na kujipinda, majasho
yakawatoka na koo likawakauka kuiga watu mashuhuri ili wasifiwe na
kufananishwa nao. Pia wenye kumwaga sifa, nao watoe sifa au pongezi zao
kwa ikhlaas na si kinafiki. Maana utawasikia wengine wakiwaendea wenye
kuwasifu na kusema ‘‘Al-Habib, si mchezo mawaidha ya leo, maana
nakwambia watu wote walikuwa wamezimia.’’ Kama vile huyo Mhadhiri
alikuwa hawaoni hao watu. Au mwengine atasema: ‘‘Muadhamu, leo ulikuwa
ukitoa kama Sheikh fulani Wallaahi’’!!
Sifa
kama hizo ambazo mtoaji anazitoa na hali anajua ni kujipendekeza tu kwa
huyo amsifiaye na kutaka aonekane mzuri, ni sifa za kinafiki na tabia
chafu ambayo hupelekea wale wenye kufanya matendo mazuri, wakaathirika
na wakawa hawafanyi tena kwa ajili ya Allaah, bali kwa kuwafurahisha hao
akina Al-Habib na kina Al-Mu'adham. Na siku zikikosekana hizo sifa,
basi huyo aliyezoea kusifiwa, anakuwa mnyonge na huenda pia ikapelekea
hata mwisho kuacha shughuli hizo za kheri kwa ajili hakuna sifa wala
kushukuriwa, au akaacha kwenda kwenye mhadhara kwa kuwa hawatokuwepo
watu wengi na hatosikika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) anasema: ‘‘Ukiwaona wale wenye kuwapa watu sifa, wamwagie vumbi usoni mwao.’’ [Swahiyh Al-Bukhaariy namba 830, na Swahiyh Muslim namba 7143].
Mwengine
ataudhiwa na watu na atasusia hata kushiriki katika shughuli hizo na
kuapa, lakini baada ya muda unamuona huyoo yuko nao tena na akiulizwa
vipi anadai aah nimeona nifanye maana haya ni maslahi ya Uislam, sasa
je, hayo maslahi ya Uislam hapo alipojitoa mwanzo alikuwa hayajui? Huko
ni kukosa Ikhlaasw. Na matendo kama hayo yanafanya mtu asiaminike pande
zote hata na hao wanaoshirikiana naye, kwani wanajua kama aliwahi kususa
basi hawezi kuacha kususa tena na huko mbeleni. Maana huyo hafanyi kwa
ajili ya Allaah bali ni kwa ajili ya watu. Kususa kunakokubalika ni pale
watu wanapokuwa katika misimamo inayopingana na Dini kama watu wa
bid'ah na wale wanaowatetea watu wa bid'ah na kushikamana nao; hao ndio
wanaopaswa kususwa kama zilipokelewa kauli nyingi kutoka kwa Mtume,
Maswahaba na wema waliotangulia kuhusiana na hilo.
Kutotaka kuwaangusha watu
Kuna
wengine wana tabia ya kuridhisha watu na kutotaka kuonekana wabaya,
hata kama itakuwa ni kufanya tendo lisilo kwa ajili ya Allaah au la
uzushi, au tendo la kheri lakini ndani yake kumekusudiwa shari. Na watu
kama hao hawataki kuwavunja wengine kwa matakwa yao, ima kwa nia ya
kujenga urafiki, au kupata maslaha fulani au kumkomoa fulani au
asichukiwe ikiwa atakataa. Kwa hiyo atafanya jambo hata kama anajua fika
ndani ya jambo hilo hakuna ikhlaas wala yeye mwenyewe haliamini kama ni
sahihi. Na wakiulizwa kwanini wanafanya jambo ambalo halina Ikhlaas
ndani yake, hutoa udhuru zaidi ya sabini.
KINGA NA NJIA ZA KUZUIA RIYAA
1. Kuongeza elimu
Mojawapo
ya kinga ya matatizo mengi yanayowakabili Waislam, ni kuongeza elimu
zaidi na sahihi kuhusu dini yao. Tunajua kuwa elimu chache ina matatizo
na elimu kubwa isiyo sahihi nayo ni msiba. Na kuwa na elimu sahihi ndipo
utakapoweza kupambanua haki na batili na yale yenye utata
yaliyofichikana, na pia ndipo utakapofikia lengo la kumcha Allaah.
Allaah kwa kulithibitisha hili Anasema: {{…hakika wanaomcha Allaah miongoni mwa waja wake ni wale Wanachuoni}} [Faatwir: 28].
Ni
muhimu kutambua kwamba, kutafuta elimu sahihi ni jukumu la kila Muislam
mwenye kumcha Mola wake, na wala si jukumu tu la Viongozi wa dini kama
Masheikh, Maimaam, Maustadh n.w. Kuna wengi miongoni mwetu
hawajishughulishi kusoma dini yao wala si jambo lililozoeleka kukuta
katika nyumba za Waislam maktaba au hata vitabu vichache muhimu vya
dini! Na sahemu nyingine kama Ulaya, utakwenda kwenye nyumba ya Muislam
ukakosa hata Qur-aan! Wengine hawajui hata Qiblah kilipo.
2. Du’aa
Katika
kizuizi na chukizo kubwa la Riyaa na kilicho chepesi kukifanya ni
du’aa. Abu Bakr Asw-Swiddiyq amemnukuu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) akisema: ‘‘Shirki iliyomo
ndani yenu inajificha zaidi kuliko mtambao wa sisimizi (si rahisi
kuonekana), na nitawaambia kitu, mtakapokifanya, basi kitawaondoshea
ndani yenu Shirki ndogo (Riyaa) na kubwa. Sema: ‘‘Allaahumma iniy a'uwdhu bika an ushrika bika wa ana a’alam, wa astaghfiruka lima la a’alam”
(maana yake: “Ee Mola wangu, naomba unihifadhi na kutomuabudu mwengine
asiyekuwa wewe (kushirikisha), na naomba msamaha kwa (kufanya) kile
nisichokijua.’’ [Swahiyh Al-Jaami’. namba 3731].
3. Kufikiri juu ya Pepo na Moto
Jambo
la tatu lenye kusaidia kumweka mtu mbali na Riyaa ni daima kuzingatia
juu ya siku ya kiama. Mazingatio ya siku ya Qiyaamah yanasaidia sana
kukuza khofu ya Jahannam, na kuongeza matashi ya kuipata Pepo. Ikiwa
mwanaadam atazingatia kuwa lengo kuu la kuishi kwake hapa duniani si
kupata umaarufu na sifa, bali ni kujilinda na adhabu ya Moto na kutaraji
kuingia Peponi, atajaribu kwa kadri ya upeo wake kujiepusha kabisa na
Riyaa. Allaah Anasema katika Qur-aan: {{… Basi anayependa kukutana na Mola wake na afanye matendo mazuri na asimshirikishe yeyote katika 'ibaadah ya Mola wake}} [Al-Kahf: 110].
Ndugu
Waislam, tujue kuwa Riyaa ni kinyume cha Ikhlaasw, palipo na Ikhlaasw
hapana Riyaa, na palipo na Riyaa hapana Ikhlaasw. Tujitahidi kutazama
nafsi zetu na kujihesabia matendo yetu tuyafanyayo kila siku, tunapotaka
kufanya tendo lolote, ni vizuri tujiulize kwanza, ‘‘Je, nafanya hili
kwa ajili ya Allaah pekee? Au kwa sababu ya fulani? Ili afurahi au
aridhike n.k. Ni tatizo ambalo si rahisi mtu kuligundua katika nafsi
yake ndio maana Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
akalifananisha na mtambao wa mdudu chungu au sisimizi.
WA ALLAAHU A'LAM
No comments:
Post a Comment