Ndugu wasomaji wa blog hii ya isspyetu baada ya kuangalia mtazamo wa wasiokuwa waislamu juu ya historia sasa tuangalie mtazamo wa waislamu juu ya historia
by Ahmed Mnungamo
Imeshabainishwa kuwa Historia, kwa ujumla, ni kumbukumbu za matendo na matukio yanayohusu maisha yote ya mwanaadamu katika jamii yake kwa muda wote uliopita
Uislamu unaitizamaje Historia ya mwanaadamu?
Mtizamo wa Uislamu juu ya historia kwa ujumla unatofautiana sana na ule wa makafiri.
Ambapo makafiri wanadai kuwa hapana Muumba wa Ulimwengu na vyote vilivyomo kwa ujumla, Uislamu unauhusisha Ulimwengu (Universe) na vyote vilivyomo akiwemo mwanaadamu, na Muumba mmoja tu Mwenye Hekima na Ujuzi usio na kikomo, ambaye ameumba kila kitu kwa lengo maalumu.
LENGO LA MAUMBILE YOTE YALIYOMZUNGUKA MWANADAMU.
Mwenyewe Muumba Allah(s.w), anabainisha lengo la kumbwa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo katika aya zifuatazo:
هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُمْ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ فَسَوَّاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ ۚ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيم
“Yeye (Allah) ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi, tena akakusudia kuumba mbingu; na akazifanya mbingu saba. Naye ndiye ajuaye kila kitu” (2:29).
وَلَقَدْ مَكَّنَّاكُمْ فِي الْأَرْضِ وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ ۗ قَلِيلًا مَا تَشْكُرُون
“Na hakika tumekumakinisheni (tumekukalisheni) katika ardhi na tumekuwekeeni humo (vitu vyote) vinavyohitajia maisha yenu. Ni shukurani chache tu mnayoshukuru” (7:10).
Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa maumbile yote ya ardhini na mbinguni(angani) yaliyomzunguka mwanaadamu, anayoyaona na asiyoyaona, yote yako pale kwa ajili ya kumtumikia na kuboresha maisha yake. Ili kufikia lengo hili, Allah(s.w) amevitiisha vitu hivi kwa mwanaadamu kwa kuviwekea sheria madhubuti za kimaumbile (natural laws):
وَسَخَّرَ لَكُمْ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِنْهُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُون
“Na amekutiisheni vilivyomo mbinguni na ardhini, vyote vimetoka kwake.”Bila shaka katika haya zimo alama kwa watu wanaofikiri (45:13).
Kisha, mwanaadamu akatunukiwa akili na vipawa vya fahamu na elimu ya kumuwezesha kuyatumikisha maumbile kwa ajili ya kuboresha maisha yake. Sayansi na teknoloia ni katika jitihada za harakati za mwanaadamu za kuyatumikisha maumbile na nguvu asili kwa ajili ya kuboresha maisha yake.
LENGO LA MAISHA YA MWANADAMU HAPA ULIMWENGUNI
Kama vitu vyote vimeumbwa kwa lengo la kumtumikia mwanaadamu, je, mwanaadamu ameumbwa kumtumikia nani?
Je, lengo la maisha ni kujipatia tu mahitaji muhimu ya maisha chakula, nguo na makazi? Mbona wanyama nao wanajitosheleza kwa mahitaji hayo hayo pamoja na kuwa hawakutunukiwa kipawa cha elimu (kujielemisha) kama mwanaadamu?
Je, ni busara kukubaliana na makafiri kuwa lengo la maisha ya mwanadamu ni lile la kutosheleza tu matashi yake ya kinyama?
Hii ni dhana tu ya makafiri kama Allah(s.w) anavyotutanabahisha:
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّار
“Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake bure. Hii ni dhana ya wale waliokufuru. Basi adhabu kali ya moto itawathubutikia wale waliokufuru” (38:27).
Bila shaka kwa wale wenye akili na busara wanayakini kuwa mwanaadamu hakuumbwa tu bure na kuletwa hapa duniani bila ya lengo lolote analotarajiwa na muumba wake alifikie.
Bila shaka mwanaadamu atakuwa na lengo la juu zaidi kuliko viumbe wengine, hasa kutokana na vipawa vya akili na elimu alivyotunukiwa kuliko viumbe wengine.
Lengo la kuumbwa mwanaadamu amelibainisha Muumba mwenyewe:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُون
“Sikuwaumba majini na watu ila tu wapate kuniabudu” (51:56).
Maana ya Ibada ni kumtumikia Allah(s.w) katika maisha yetu yote.
Kumtumikia Allah(s.w) ni kumfanya Allah(s.w) kuwa ndiye Bwana (Rabb) wetu pekee ambaye ndiye pekee tunayepaswa kumtii kwa unyenyekevu kwa kufuata barabara mwongozo wa maisha aliyotuwekea.
Utiifu na unyenyekevu wetu kwa Allah(s.w) utadhihiri pale tutakapopania kwa moyo mkunjufu kutenda yale yote aliyotuamrisha na anayoyaridhia na kujiepusha mbali kutenda yale yote aliyotukataza na yanayomchukiza katika kuendea harakati za maisha yetu yote ya kila siku.
Ibada kwa mtizamo huu inamuhusu kila mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Ili kila mtu amuabudu Allah(s.w) inavyostahiki, jamii inawajibika kuweka mazingira ya kumuabudu Allah(s.w) katika kila kipengele cha maisha kwa muda wote kwa kuunda dola yenye mamlaka kamili ya kuamrisha mema yanayoleta furaha na amani katika jamii na kukataza na kuyatokomeza maovu yanayoleta huzuni na vurugu katika jamii.
No comments:
Post a Comment